Enyi mlio amini! Yanapo mfikia mauti mmoja wenu na akataka kutoa wasia, basi wawepo mashahidi wawili miongoni mwenu ambao ni waadilifu. Na mnapo kuwa safarini, na msiba wa mauti ukakusibuni, basi washuhudie wengineo wawili wasio kuwa katika nyinyi. Mtawazuia wawili hao baada ya Sala na waape kwa Mwenyezi Mungu, mkitilia shaka, wakisema: Hatutopokea thamani yoyote kwa haya hata kwa ajili ya jamaa; na wala hatutaficha ushahidi wa Mwenyezi Mungu; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi.