Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.